MIGOGORO ni jambo la kawaida katika uhusiano wa kimapenzi au ndoa. Na ndiyo maana hata kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au ndoa si jambo la kushangaza katika jamii. Mahusiano hayavunjiki hivi hivi, zipo sababu.
Ukizifahamu sababu za kuvunjika kwa mahusiano, kama wewe ni mwathirika wa kuvunjika kwa uhusiano utapona haraka na kujifunza kupenda tena. Kwako wewe ambaye uhusiano wako na mwenzako haujavunjika, au labda hata hujawahi kuingia katika uhusiano, unapozifahamu sababu za kuvunjika kwa uhusiano itakusaidia kufahamu jinsi ya kuenenda unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa, kwa mustakabali mwema
wa uhusiano wako na mwenzako.
Kati ya shughuli nzito ambazo huwakumba watu walio katika mahusiano ya kimapenzi au ndoa ni kuhakikisha kuwa mahusiano yao yanakuwa imara. Ni shughuli yenye changamoto nyingi kwani huhitaji uwiano, maana mwanamume na mwanamke wameumbwa tofauti na kila mmoja ana matakwa na matarajio yake.
Sababu za kuvunjika kwa uhusiano zinaweza kuwapo nyingi na kutofautiana kutoka uhusiano huu na ule, lakini zipo kumi ambazo zinaweza kuchukuliwa kuwa kuu. Ukizifahamu utajua jinsi ya kuboresha uhusiano wako wa sasa au baadaye, au kukuweka sawa kisaikolojia kwa ajili ya uhusiano mpya.
Sababu zenyewe ni hizi zifuatazo: -
1. KUKOSEKANA KWA UAMINIFU
Kushindwa kutimiza ahadi, kusema uwongo au kufanya usaliti wa kimapenzi ni mambo
ambayo humwondolea mtu uaminifu kwa mwenzake. Kwa hakika, kukosekana kwa uaminifu ni sababu kuu ya kuyumba na hata kuvunjika kwa mahusiano yaliyo mengi.
Iwapo kuaminiana kwa msingi kabisa katika uhusiano kutavunjwa mara kwa mara, hasira za mpenzi kwa mwenzake zitalimbikizwa na hamu ya wapenzi/wenza kuendelea kuishi pamoja itapungua. Wapenzi walio katika uhusiano wenye mizizi na afya njema wanaweza kukubaliana kumaliza tofauti zao na kusonga mbele. Kama wataheshimu ahadi na viapo vyao vipya mambo yataendelea.
Kumdanganya mpenzi mara kwa mara, kumsaliti mara kwa mara na kuvunja ahadi zako mara kwa mara huufanya uhusiano kudhoofika na hatimaye nguzo yake muhimu – yaani kuaminiana – kuanguka. Hapo ndipo uhusiano hufika kikomo.
2. KUTOKUWEPO KWA UWIANO WA MADARAKA
Katika zama hizi ambapo wanawake wamezifahamu haki zao, kutokuwepo kwa uwiano mzuri katika kutoa maamuzi inaweza kuwa sababu mojawapo ya kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa.
Inapotokea kuwa mmoja tu ndiye anayetoa maamuzi kuhusiana na shughuli mbalimbali, uchaguzi wa marafiki, masuala ya kifedha, masuala ya nyumbani, likizo na kadhalika, mwingine anaweza kujiona kama vile hana nafasi katika ushirika huu, hivyo kuamua kujitoa.
Katika zama hizi, wanawake wengi wanafundishwa kuwa na hisia za usawa. Iwapo itatokea mmoja wa wanandoa au wapenzi akajihisi kuwa ametengwa katika maamuzi ya msingi yakiwamo yale yanayohusiana na mustakabali wa maisha yake, ni rahisi sana uhusiano kufika kikomo.
3. KUSHIKILIA IMANI POTOFU
Katika jamii kuna imani potofu mbalimbali kuhusiana na wanawake na wanaume.
Mathalani, kuna imani kuwa wanaume ndio hupenda sana ngono kuliko wanawake au kwamba wanawake ni watu wa kusikiliza na kupelekeshwa tu.
Iwapo mmoja wa wanandoa au wapenzi ataamini katika mojawapo ya imani hizi potofu zenye msingi wa mfumo dume, au imani nyingine zozote, kuna uwezekano mtu huyu akajenga matarajio yasiyokuwa halisi – jambo ambalo hujenga uwezekano mkubwa wa kushindwa kwa uhusiano. Hapa pia kitachotakiwa ni uwiano wa nguvu kutoka pande mbili na kuepuka kuamini katika imani potofu.
4. KUMTENGA MTU NA WATU WAKE
Mojawapo ya sababu kuu za kuachana kwa wapenzi ni mmoja kujihisi ametengwa na
marafiki zake aliotoka nao mbali, ndugu, jamaa na wanafamilia wake, kwa kizingizio
cha mapenzi.
Mara nyingi, wapenzi hujitenga na watu wao wa karibu kutokana na hofu na
kutokujiamini, lakini uhusiano wa aina hii hauwezi kuwa na nguvu na unaweza kujenga mazingira ya kuibuka kwa matatizo mengine ambayo hatimaye yatauua uhusiano.
5. KUTOJITAMBUA KWA MPENZI
Iwapo itatokea kuwa mmoja wa wapenzi/marafiki au wote wawili akawa hajitambui na kufuata matakwa yake, mahitaji yake, matamanio yake, mipango yake ya baadaye, malengo yake, msimamo wake, hulka yake na vipaumbele vyake, haitakuwa rahisi kwa watu hawa wawili kuwa na uhusiano wenye afya.
Kujitambua huwasaidia wapenzi kuwa huru kila mmoja kwa mwenzake, akimweleza anataka nini, jambo ambalo husaidia kuimarisha uhusiano. Lakini inapotokea kuwa mmoja wa wapenzi hajitambui, au wote wawili hawajitambui, ni rahisi sana uhusiano kuvunjika, hasa kama wahusika waliingia katika uhusiano huo wakiwa na umri mdogo.
6. KUTOJITHAMINI NA KUTOJIAMINI
Inapotokea mmoja wa wapenzi akajihisi kuwa hastahili kupendwa, hiyo inatosha kuwa sababu ya mazingira ya kuvunjika kwa uhusiano. Hali hii hutokana na kutojithamini na kutojiamini kwa mtu – mambo ambayo yanaweza kusababishwa na sababu mbalimbali yakiwamo malezi.
Kutokujiamini au kuwa na hofu ya kuachwa kunaweza kumfanya mtu ambane sana mwenzake na kumnyima uhuru – jambo ambalo halifai kwa afya na ustawi wa uhusiano. Kujiamini na kujithamini kwa mwenza ni njia mojawapo ya kuepuka kuvunjika kwa uhusiano.
7. WIVU ULIOKITHIRI
Wivu ni mojawapo ya sababu kuu za kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa. Wivu wa kupindukia unaweza kusababisha ugomvi ambao nao ni sababu kubwa ya kuachana kwa wapenzi.
Wivu husababishwa zaidi na kutokujiamini kwa mtu. Kwa hiyo, ili kuepuka wivu na
kuunusuru uhusiano wa kimapenzi, lazima mtu kwanza ajithamini na kujiamini kuwa
anastahili kupendwa na mpenzi wake kama alivyo.
8. MAWASILIANO HAFIFU
Mawasiliano ni kitu muhimu sana katika mapenzi. Iwapo wapenzi watashindwa kuelezana hisia zao, mawazo yao, mitazamo yao, imani zao, matatizo yao au hata furaha zao, uhusiano utakuwa unaelekea pabaya.
Inapotokea hiyo ikawa sababu ya kuachana kwa wapenzi, basi mtu anapojifunza tena
kupenda atapaswa kujifunza pia jinsi ya kuwasiliana vema na mwenzake, kwani kwa
hakika mawasiliano mabaya ni sababu kubwa ya kuachana kwa wapenzi.
9. MMOJA KUMDHIBITI MWENZAKE
Inapotokea kuwa mmoja wa wapenzi anataka kumdhibiti mwenzake na kumwendesha mithili ya mtu anayemwendesha farasi, uhusiano unaohusika utakosa mapenzi – na hiyo itakuwa sababu kubwa ya kuachana kwa wapenzi hawa baadaye.
Sababu hii inaweza kuchukuliwa katika namna tofauti. Mtu anaweza kumbana mwenzake kwa kumfuatilia muda wote, kumtishia – mathalani anapochelewa nyumbani au kwenye miadi – na kutompa ruhusa na uhuru wa kupanga ratiba zake au kutoka na watu wa karibu naye. Hii si tabia ya kimapenzi na matokeo yake ni kushindwa kwa uhusiano.
10. UNYANYASAJI
Hii ndiyo sababu ambayo pengine iko wazi zaidi. Kuna aina mbalimbali za unyanyasaji
ambao hujitokeza baina ya wapenzi na si lazima kwamba mwanamume ndiye anayemnyanyasa mwanamke kama ilivyozoeleka. Hata wanawake huwanyanyasa wanaume.
Unaweza kudhani ukinyanyaswa tu na mpenzi au mwenza utamwacha, lakini ukweli ni kwamba wengi huvumilia, pengine kutokana na kuiogopa jamii inayowazunguka. Lakini ukweli ni kwamba unyanyasaji huondoa kabisa maana ya mapenzi na kusababisha wapenzi
wengi kukosa sababu ya kuendelea kuwa pamoja.
KUWA MAKINI
Migogoro ni kitu cha kawaida katika uhusiano wa kimapenzi – na kwa hakika haiepukwi, isipokuwa wenza hujifunza jinsi ya kuimaliza na kuondoka wakiwa salama. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo uhusiano hufikia kikomo. Una heri wewe ambaye umezifahamu sababu kuu za kuvunjika kwa uhusiano maana zitakusaidia kufahamu jinsi ya kujipanga na kutengeneza uhusiano wenye afya na mustakabali mwema.
No comments:
Post a Comment