Friday, May 18, 2012

Sababu za Vijana Kujingiza katika Tabia za Hatari na Namna ya Kuwasaidia

Katika makala hii tunashirikisha namna ya kuwasaidia vijana ili waweze kuvuka vikwazo vinavyoweza kuwafanya wasifikie malengo waliojiwekea maishani mwao. Tunatambua kwamba, yapo mambo mengi yanayoweza kuwachelewesha au kuwakwaza vijana kutofikia malengo yao ya maisha.

Baadhi yake ni kama:

Dawa za kulevya Ulevi VVU/Ukimwi Mimba kabla ya wakati, n.k. Katika makala hii, tunaelezea sababu chache zinazopelekea vijana (wasichana) kupata mimba kabla ya wakati. Pia tunapendekeza namna ya kuweza kuwasaidia ili wasijikute katika mtego huu na pia waweze kufikia malengo yao katika maisha yao. Ingawa sababu hizi zinawalenga wasichana moja kwa moja, hata hivyo zinaweza kutumika kwa wavulana pia, kwa vile wavulana wanajiingiza katika mambo haya kirahisi kuliko wasichana. Bi. Tricia M. Davis amefanya utafiti kati ya wasichana wapatao 500 wenye umri wa miaka chini ya 19, waliowahi kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika utafiti wake anaeleza sababu saba zilizojitokeza na kuchangia katika hawa kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika makala yake, “An Examination of Repeat Pregnancies Using Problem Behaviour Theory”, iliyochapishwa katika Jarida la Journal of Youth Studies (Vol. 5,no.3, 2002, pp.337-351), anafafanua kwa kina juu ya tatizo hili. Hivyo tunaamini kuwa baada ya kupitia maelezo haya, kama walezi wa vijana tutakuwa na upana wa mawazo na kuwawezesha vijana namna ya kupanga malengo mazuri katika maisha yao na jinsi watakavyoweza kuyafikia malengo hayo.

1. Kutokuwa na Malengo ya Maisha Sababu ya kwanza, kati ya saba zilizoorodheshwa ni kutokuwa na malengo maalum katika maisha. Vijana wenye malengo endelevu katika maisha huwa wanachelewesha tendo la ndoa na hivyo kutopata mimba kabla ya wakati. Kijana anapokuwa amejiwekea malengo makubwa katika maisha yake, hakika atakuwa makini zaidi na daima atajiepusha na tabia zinazoweza kumpelekea kutofikia malengo yake. Kwa mfano, ikiwa kijana fulani aliye katika kidato cha kwanza (Form I) na ana lengo la kuwa rubani wa ndege au kiongozi mashuhuri katika nchi au mtu yeyote maarufu, ni wazi atajishugulisha zaidi na mambo ya masomo. Hali hii haina maana kwamba hatajihusisha na starehe zinazoambatana na ujana! La hasha. Ila hata kama anakwenda disko basi atatambua lengo lake na atajua dosari inayoweza kumpata endapo atajilegeza na kufuata vishawishi vya ndani ya disko. Kwake atatambua kirahisi kuwa akifanya ngono anaweza kupata mimba na hivyo kushindwa kufikia malengo yake. Msichana mwenye lengo kuu kama hili ni tofauti na yule asiyekuwa na malengo. Msichana asiyejua la kufanya baada ya kumalizia shule ya msingi ni rahisi kwake kujiingiza katika tabia za hatari. Hali halisi ya vijana wengi wa Afrika Mashariki ni kuwa hawana uhakika na maisha baada ya shule ya msingi. Kwa hiyo, sisi ambao tunahusika na malezi ya vijana tutambue kwamba njia rahisi ya kuwawezesha vijana kutokupata mimba, wala kujiingiza katika tabia za hatari, haitoshi kuwaambia “muwe wazuri”, bali kuhakikisha kuwa wanaweka malengo makuu katika maisha yao.

2. Kutojithamini ya Kutosha Hii ni hali ya kijana kujiona hafai kwa chochote katika familia anamotoka au katika jamii ya watu inayomzunguka. Hisia hii inampelekea kujichukia na kupata msukumo wa kutaka kutafuta thamani ya nafsi yake kirahisi. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kujaribu mambo ya mapenzi. Kwa msichana wa hali hii ni rahisi kufikiri thamani yake inatokana na tendo hili la ngono kwani linaambatana na lugha nzuri wanazotumia wavulana na ahadi au zawadi anazoweza kupewa. Wasichana wanaotoka katika familia zisizo na upendo wa kweli kati ya wazazi (baba na mama) ni rahisi kudanganyika na kutafuta thamani zao nje ya familia. Au mzazi hasa baba, anayetumia lugha ya ukali daima au lugha ya mfumo dume humfanya binti kutojisikia wa thamani. Na hali ile ya kupendwa inapokosekana nyumbani, basi ni wazi msichana huyu anapokutana na mvulana mwenye maneno matamu anaweza kudanganyika kirahisi. Pia misamiati kama, “kulizaliwa kwa bahati mbaya” na nyingineyo inaweza kupelekea kwa binti kutojipenda. Ikumbukwe kwamba nyumbani ni shule ya kwanza ambapo kila mmoja wetu anajifunza maana ya utu na namna ya kupenda na kupendwa na wengine. Kwa upande wa msichana, baba ndiye mwanamume wa kwanza anayetokea kuhusiana naye, hivyo ana jukumu la kujenga thamani ya huyu binti anayekua. Hivyo ni dhahiri kwamba kama tunapenda kuwasaidia vijana kutokupata mimba kabla ya wakati, ni bora kuhakikisha kama kijana fulani anathamini utu wake. Tunaweza kuwasaidia vijana kwa kuandaa semina zinazohusu kujitambua na kuwasaidia kuanza safari ya kutafakari, “Mimi ni nani?,” na “Thamani yangu inatokana na nini?” Hii itawasaidia kutambua kwamba thamani ya mtu haitegemei watu wengine wala wanavyosema, hata si umbo alilo nalo, bali ni hali ya ndani. Thamani ya mtu ipo ndani ya utu wake, yaani nafsini mwa mtu mwenyewe.

3. Kutowajibika Sababu nyingine inayoweza kumpelekea kijana kupata mimba kirahisi ni kutokuwa na tabia za kuwajibika (External locus of control). Kutowajibika kuna maana ya mtu anavyoeleza matukio mbalimbali ya maisha yake na jinsi gani anavyojiepusha na tukio lile. Tabia hizi zaweza kuonekana hata katika mambo madogo madogo. Kwa mfano, kijana akidondosha kitu fulani na kusema, “Kitu hiki kimedondoka”, yeye anajaribu kutafsiri tukio lile kuwa hakuhusika nalo kabisa. Au mwingine anapovunja glasi na kusema, “Glasi imevunjika” anajaribu kutowajibika na tukio hilo. Sote tunatambua jinsi Adamu alivyotaka kujiepusha na kutokuwajibika kwa kosa alilofanya katika bustani ya Edeni. Mungu alipomuuliza, “Umefanya nini?” Adamu alimjibu Mungu, “Mwanamke uliyenipa ndiye alinidanganya nami nikala…” Adamu hakutaka kuwajibika na tendo lake. Hali kadhalika kijana mwenye mazoea ya kutowajibika katika mambo madogo madogo, ni rahisi kwake kujiingiza katika ngono na hatimaye kupata mimba bila kujali au kuwajibika. Wasichana wenye tabia ya kusema, “Shetani alinidanganya” au “Tulikuwa tunajaribu,” wanaonyesha dalili za kutowajibika na tendo walilofanya. Ni dhahiri kwamba msichana wa namna hii hajajifunza kutokana na kosa la mwanzo, hivyo ni rahisi kwake kurudia kitendo hicho hicho. Sisi kama walezi wa vijana tunahitaji kuanza kuwazoesha vijana tulio nao kuwajibika katika mambo madogo madogo. Kupendekeza kwa wazazi, walezi, na vijana wenyewe kwa kuwapa nafasi za kujaribu shughuli zinazoendana na umri wao, na hasa katika kumiliki vitu vyenye thamani ndogo. Hii itawafanya kujisikia kuwa wenye kuchukua hatamu ya maisha yao.

4. Ukosefu wa Uchaji Ukosefu wa uchaji ni ile hali ya kijana kutojali mambo ya kiimani. Vijana wanaokuwa na hali hii ya kutojali mambo ya kidini na imani kwa ujumla wanajiweka katika mazingira rahisi zaidi ya kujiingiza katika tabia za hatari. Hii ni kwa sababu wanakuwa wamezamisha dhamiri zao zisiwasumbue wanapokuwa wamekosea. Kwa upande mwingine, vijana wanaojihusisha na vikundi mbalimbali vya kukuza imani, wanapata malezi mazuri juu ya dhamiri zao na hivyo hata kama wakikosa ni rahisi kwao kurudi katika msingi mzuri wa maadili. Vikundi hivi ni kama vile vya kutafakari Neno la Mungu, fokolare, vikundi vya kiutume na vinginevyo. Uchaji hapa si kuja kanisani Jumapili kama sheria fulani, bali ni ile hali ya kuguswa na Mungu; kuwa na mang’amuzi binafsi ya upendo wa Mungu. Uchaji hapa si tendo la kurudia rudia sala fulani, bali ni hali ya kutafakari na kujiweka katika hali ya kuunganika na Mungu. Vijana wenye mazoea haya wanajenga polepole ndani yao uwezo wa kuchunguza dhamiri na kutathmini siku ilivyokuwa kabla ya kulala (Examination of coscience). Hata katika sala binafsi wanaweza kugundua kosa dogo walilolifanya katikati ya siku bila wao kujua kwa sababu ya mahangaiko ya maisha. Hali ya namna hii inaweza kutumika kama kinga kwa makosa makubwa kama tabia za hatari tunazozizungumzia katika makala hii. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kupendekeza mpango fulani utakaohakikisha vijana wanapata fursa ya kujituliza na kutafakari maisha yao ya kiroho. Katika matoleo ya Mlezi yaliyopita, tumewahi kuzungumzia juu ya maisha ya kiroho kwa vijana. Tunaweza kurejea na kuona namna gani tunaweza kuwa na mpango utakaowasaidia kuanza safari hii ya kuwa na uchaji.

5. Mazingira Duni ya Nyumbani Hii ni sababu nyingine inayoweza kuwapelekea vijana kujiingiza katika tabia za hatari. Kama msichana anaishi na mzazi mmoja, kuna uwezekano wa binti kupata mimba mapema kutokana na kuathiriwa na mfano wa muundo wa familia anayoishi. Pia kwa wale wanaotoka katika familia ambazo mume na mke si waaminifu, kuna uwezekano mkubwa wa kijana kushawishika na kuanza mambo ya mapenzi mapema. Hata hivyo, vijana wanahitaji kusaidiwa namna ya kuzipokea familia zao, na kuamini kuwa si lazima waige mfano potovu wa wazazi wao. Zaidi ya hayo, ni kutambua kwamba kuna mambo wanayoweza kuyabadili na mengine wanahitaji kukubali nayo. Ni lazima vijana wajue hawawezi kutawala tabia za wazazi wao ila wanaweza kukabili tabia zao wenyewe. Kwa kufanya hivyo wanakuwa mashujaa wa mazingira magumu waliyojikuta nayo.

6. Mshinikizo wa Rika Mshinikizo wa rika unaweza kuwalazimisha vijana lakini si kwa sehemu kubwa! Vijana wanaweza kushawishika kufanya ngono au kujiingiza katika tabia za hatari kutokana na hadithi zinazosimuliwa na wenzao. Kila mmoja hujidai kuwa alijaribu mambo haya na kuelezea jinsi alivyojisikia. Hali hii inaweza kuchochea hamu ya kutaka kujaribu mambo yale ya hatari. Kama kijana tayari ana malengo na anajithamini si rahisi sana kupeperushwa na upepo huu wa masimulizi haya. Lakini kama kijana hana malengo maalum katika maisha na hajui thamani yake, basi ni wazi mshinikizo wa rika una nafasi kubwa ya kumpotosha.

7. Tabia ya Kupenda kujaribu mambo mapya Vijana wenye tabia ya kupenda kujaribujaribu ili kujua ladha yake hata bila kujali madhara yake wanaweza kuingia katika mtego kirahisi. Kwa kufikiri kuwa wanaweza kujaribu tendo lolote la hatari mara moja tu na kuacha, kumbe kunaweza kuwa mtego wa kudumu. Hata mara moja inaweza kuwa mara nyingi. Kuna methali ya Kiswahili inayosema, ‘Mwonja asali haachi kuchonga mzinga.’ Vijana wanatakiwa kueleweshwa kuwa kila tabia inaanza kwa tendo moja la awali.

Hitimisho Sababu zilizotolewa hapa juu zinaweza kutumika kama kinga ya kuwasaidia vijana kutojiingiza katika tabia za hatari – kama vile utumiaji wa madawa ya kulevya, ulevi, na kupata mimba kabla ya wakati. Basi, vijana wasaidiwe kuwa na… Malengo ya maisha Hali ya kujithamini Tabia ya kuwajibika Uchaji Uwezo wa kutokuzamisha na mazingira duni ya nyumbani Msimamo wa kutofuata mkumbo, na Uvumilvu wa kutoanza tendo lisiloendana na hali ya maisha.